NI WAKATI WA UCHUMI,BIASHARA NA UJASIRIAMALI. Kila mwaka Tanzania inazalisha wahitimu wa shahada ya kwanza wasiopungua 40000, wale wanaosoma vyuo vya ndani na vyuo vya nje. Maana ya idadi hiyo kubwa ya wahitimu ni vita ya kutafuta ajira ambayo inaishia wahitimu kutembea na bahasha za vyeti kila ofisi bila matumaini ya kuajiriwa.
Kama hiyo haitoshi hata wale ambao wanapata bahati ya kuajiriwa wanakuwa na wakati mgumu sana kutoa ushirikiano kazini kwani inawapasa kufundishwa upya namna ya kufanya kazi kwani vyuo vingi barani Afrika vinafundisha nadharia na si vitendo kitu kinachowagharimu sana wasomi wapya.
Nchi zilizoendelea ziligundua changamoto hii karne nyingi sana tangu miaka ya 1700, ndipo wakaja na wazo la ujasiriamali. Lengo likiwa ni kumfanya mhitimu kujiajiri mwenyewe bila kufikiria kuajiriwa.
Wachumi barani Afrika mbali ya kuipokea dhana ya ujasiriamali bado wanaumiza vichwa kuhusiana na dhana hii ili kuweza kuipatia tafsiri ya moja kwa moja.
Hata sasa ukienda mitaani kuuliza watu maana ya ujasiriamali utapata tafsiri zaidi ya elfu moja. Hakuna mtu ambae atakueleza kitu cha kunyooka. Maana yake bado elimu ya ujasiriamali haijasambaa katika vichwa vya watanzania. Wachumi wanasema ujasiriamali ni hali ya mtu kuthubutu kuanzisha kitu kipya katika biashara ili aweze kupata faida baadaye.
Kwa lugha ya kibiashara mjasiriamali ni mbunifu ambae hunadi ubunifu wake kwa vitendo kupitia bidhaa anazouza ama huduma anazotoa kwa njia mpya ya uzalishaji pesa sokoni.
Hapa ndipo panapochanganya watu wengi, utaweza vipi kubuni kitu kipya ambacho hakipo katika jamii. Watanzania wengi wanaonekana wavivu kwa kushindwa kuzitumia elimu zao vyema. Maana ukimwambia mwanafunzi aliehitimu shahada ya biashara aanzishe biashara atakwambia nianzishe biashara gani wakati kila biashara ninayoifikiria tayari imeshashamiri katika soko.
Nilipokuwa masomoni, mwalimu wangu wa somo la ‘micro economics’ alipata kusema akiwa darasani kuhusu ujasiriamali;
Alisema “Mjasiriamali ni yule anaeleta mageuzi au mabadiliko katika soko na kuwajibika katika bidhaa au huduma anayofanya kwa kutafiti mazingira ya biashara au huduma kabla hajaamua kutoa pesa zake mfukoni kuwekeza katika shughuli hiyo ya kijasiriamali.”
Kitu nilichojifunza kutoka kwa mwalimu huyu wa uchumi ni kuwa watu wengi wanakosa nafasi ya kutafiti mazingira ya biashara kabla hawajaamua kutoa akiba yao ama mtaji.
Utaona watu wengi wanapata pesa nyingi lakini ukiwaambia waanzishe biashara haichukui muda atakwambia biashara ni mbaya na pesa zote zimeisha, kibaya zaidi atakwambia mbali ya pesa kuisha lakini bado anadaiwa.
Kwa sasa ujasiriamali unafundishwa katika ngazi nyingi za elimu kuanzia sekondari mpaka vyuo, lakini hakuna mabadiliko yoyote yaliyofanyika katika sekta ya ajira. Unaweza kujua sababu?
Hao waalimu walioteuliwa kufundisha somo la ujasiriamali wenyewe hawaamini katika ujasiriamali. Hapo ndipo tatizo lilipo, hakuna siri.
Utashangaa kuona na kufundishwa na mwalimu wa somo la ujasiriamali wakati yeye mwenyewe hana biashara hata ya kuuza mkaa, hajaonyesha mafanikio yoyote katika kitu anachokifundisha. Maana yake hawezi kutoa mifano hai kwa wanafunzi wake na hicho kinawafanya wanafunzi waamini wanachofunzwa ni somo tu kama yalivyo masomo mengine.
Hakuna uzito wowote unaochukuliwa na wanafunzi wa somo la ujasiriamali, hiki ni kikwazo na kunahitaji kufanywa utafiti kuona ni namna gani masomo ya ujasiriamali kwa baadhi ya vyuo na shule za sekondari yameleta mafanikio kwa wanafunzi tangu kuanzishwa utaratibu huo.
Mwalimu aliendelea kutueleza dhana ya ujasiriamali kuwa ni “Kwa yeyote anaetaka kuwa mjasiriamali ni lazima awe na mapenzi ya biashara ama huduma anayotoa, asifuate mkumbo kwa sababu tu biashara anayotaka kuifanya ni maarufu katika eneo analoishi.
“Bali mtu ajikite kwa dhati na tija ili kupata kipato katika maisha yake la muhimu ni nia ya dhati na kujitoa akubaliane na changamoto zozote atakazokutana nazo maana biashara unapoanza ni ngumu na hakuna faida ya haraka labda iwe ni biashara ama huduma ya haramu.”
Watu wengi wanashindwa katika ubunifu, utakuta biashara imeanza vizuri na maendeleo ni mazuri, lakini haonyeshi mabadiliko ama ubunifu ili kuweza kuwavutia wateja wake.
Usafi katika eneo la kazi, mavazi ama sare za watoa huduma, zawadi na ahadi ndogondogo kwa wateja wa kila siku ama kauli nzuri pia ni kitu muhimu sana kwa mjasiriamali. Hakuna kitu kibaya kama kuwa na kauli mbaya kwa wateja hasa wateja wa zamani, mtu asiridhike kwa kusema hawa ni wateja wangu hakuna sehemu nyingine watakayopata huduma nzuri kama hapa, waonyeshe kwa vitendo kuwa wewe ndie kimbilio lao na si kujisifu tu.
Katika suala la mtaji mwalimu alieleza kuwa “Kuanzisha biashara ni suala la maamuzi, ni lazima uhakikishe unakipenda kile unachokifanya na uwe na njaa ya mafanikio.
“Watu wengi pesa ndiyo wanaita mtaji, lakini kwangu mtaji ni shauku ya kufanikiwa na ndicho kitu kitakachofanya biashara yako ikaendelea na kuleta mafanikio makubwa. Mathalani umepanga kupata 1,000,000/= kwa mwaka na baada ya mwaka ukapata 500,000/= halafu ukasema inatosha. Ni lazima ujiulize umeshindwa vipi kutimiza malengo yako,”
Mafanikio yana njia nyingi, usiridhike na hatua uliyofikia, elimu ni kila kitu. Usisite kujiendeleza kielimu na kujua zaidi kuhusu biashara ama huduma unayotoa.
Mjasiriamali hana wivu mbaya bali ana wivu wa kimaendeleo kwa kutembelea ofisi za washindani wake kibiashara na kujua siri za mafanikio yao badala ya kukaa na kunung’unika tu kuwa mambo hayamuendei vizuri.
Wapo watu wanaamini tofauti kubwa ya pengo kati ya maskini na tajiri ni elimu ya ujasiriamali. Maana ya imani hii ni kuwa maskini wengi wanashindwa kuendesha biashara kwa kuwa hawana elimu ya ujasiriamali ama kwa kuipata darasani ama kwa kuona.
Matajiri wengi duniani hawana elimu kubwa, waliacha shule wakiwa wadogo ama walishindwa kumaliza elimu ya chuo kwa kuelekeza nguvu zao katika kutafuta pesa.
Hii maana yake ni kuwa haihitaji kukaa darasani kujifunza ujasiriamali, bali hata kwa kukaa na watu wanaojua elimu hii unaweza kujifunza kwa vitendo. Lakini tatizo kubwa tulilonalo kwa sasa nchini mwetu ni namna gani tutawasaidia wahitimu wanaotangatanga mitaani bila kazi.
Dhana ya ujasiriamali katika akili za watu inabaki kuwa ni biashara. Lakini hata huduma inaweza kuwa ni ujasiriamali. Maana si wanafunzi wote wanaomaliza vyuo ni wahitimu wa shahada ama stashahada za elimu ya biashara. Bali kuna wanafunzi ambao wamesoma computer, maendeleo ya jamii, utawala na mawasiliano ya umma ama uhandisi.
Hivyo kinachopasa kufanywa na serikali kwa sasa ni kuhakikisha wanatoa elimu ya ujasiriamali kwa wanafunzi waliohitimu na si wanafunzi ambao bado wapo vyuoni. Maana wengi hugundua umuhimu wa masomo kama hayo mara wamalizapo shahada zao.
Masomo ya ujasiriamali huonekana kama masomo ya kujazia vyeti hayachukuliwi kwa uzito wake. Mwanafunzi aliehitimu shahada ya uongozi atakwambia mimi ujasiriamali utanisaidia nini, lakini hajui kama anaweza kufungua ofisi na kutoa huduma zinazotokana na masuala ya uongozi wa umma na kupata ajira bila kutegemea Serikali kumpa ajira.
Yote haya hayafunzwi ama yanafunzwa lakini wanafunzi hawayachukulii kwa uzito wake. Kimsingi elimu ya ujasiriamali ndiyo mkombozi wa tatizo la ajira kwa nchi zinazoendelea.